Uganda imekosoa tahadhari iliyotolewa na Marekani iliyodai kuwa ni hatari kufanya biashara na kuwekeza katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Godfrey Kabbyanga, Waziri Msaidizi wa Habari wa Uganda amewataka wawekezaji wapuuze tahadhari hiyo ya Marekani akisisitiza kuwa, maonyo kama hayo hayaendani na hali halisi katika nchi hiyo ya Afrika.
Juzi Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilichapisha waraka wa tahadhari, ikiwaasa watu wenye nia ya kwenda kuwekeza nchini Uganda kughairi azma zao eti kutokana na kushamiri ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waziri Msaidizi wa Habari wa Uganda amebainisha kuwa, hii si mara ya kwanza kwa Marekani kutoa onyo la kichekesho dhidi ya Uganda, lakini pamoja na hayo, Uganda haijaporomoka, bali imeendelea kuimarika hata zaidi.
Mapema mwaka huu, Washington ilitoa onyo jingine lililowataka watu hasa Wamarekani wasisafiri kwenda Uganda, muda mfupi baada ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda kupasisha sheria ya kupambana na ushoga.
Uganda imekuwa ikivutana na nchi za Magharibi tangu ipasishe sheria hiyo kali ya kukabiliana na vitendo viovu vya ubaradhuli, ushoga na maingiliano haramu ya watu wa jinsia moja.