Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko kushughulikia upatikanaji wa nishati ya mafuta kwenye maeneo yote nchini ili Watanzania wote wapate huduma hiyo.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Bungeni Dodoma leo September 07, 2023 wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu ambapo Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi alitaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha Taifa linakuwa na mafuta muda wote na yanapatikana kwa bei ambayo Watanzania wote wataimudu.
Waziri Mkuu Majaliwa ameelekeza pia wakati wakishughulikia suala hilo wapanue wigo wa Waagizaji wa mafuta ili kuwepo kwa mafuta mengi nchini kwa usalama wa Taifa.