Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema uhalifu wa mitandaoni umeendelea kupungua kutokana na mikakati inayofanywa na serikali, ikiwamo kuanzisha mfumo wa namba maalum ya kupokea na kuzifungia laini zinazobainika kufanya utapeli.
Akijibu maswali hayo, Waziri Nape amesema kazi ya TCRA si kukamata wahalifu bali kuwezesha polisi kupata ushahidi wa kuwapata wahalifu.
Nape ameyasema hayo bungeni jana alipojibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Buhigwe (CCM), Kavenjuru Felix. Mbunge huyo alitaka kauli ya serikali kutokana na wizi wa mtandaoni kuendelea na sababu za kutokamatwa wahalifu hao ilhali laini zinasajiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na polisi wanaruhusiwa kuchukua taarifa zozote za laini zilizosajiliwa.
Amesema TCRA ina jukumu la kufungia laini na kwa Septemba 2023 kulikuwa na laini za uhalifu 23,328 na zilipungua hadi kufikia 21,000 mwezi Desemba mwaka huo.
Amesema kuwa hadi Machi 2024 kulikuwa na laini za simu 17,318 huku akidai walipoanza uhakiki kulikuwa na laini milioni 9.045 ambazo hazijahakikiwa na walifungia laini 907,046.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alihoji mkakati wa serikali kukomesha wizi wa mtandaoni; naye Waziri Nape akijibu swali hilo, alisema serikali tayari imechukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuweka mazingira salama kwa wananchi hususan kwenye mitandao.
“Mwaka 2015, serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao, pia kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo,” amesema.