Uhusiano wa kiuchumi baina ya mataifa umeelezwa kuwa ndio uhusiano imara na bora zaidi ukilinganisha na nyanja nyingine za uhusiano duniani kwa sasa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Czech, Mhe. Jan Lipavský wakati wanazungumza na waandishi wa habari jijini Prague Januari 17, 2025.
Waziri Kombo amesema kuwa Tanzania na Czech zina uhusiano mzuri na imara wa kidiplomasia ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo tokea miaka ya 60 na kwamba jukumu walilo nalo ni kuhakikisha kuwa uhusiano huo unaimarishwa na kuboreshwa ili uendane na mahitaji ya sasa ya kiuchumi.
Waziri Kombo ambaye alikuwa nchini Czech kwa ziara ya kikazi ya siku tatu amesema ziara yake nchini humo ambayo ni ya kwanza kwa Mwaka 2025 inaonesha dhamira ya dhati kwa Czech na kutoa ujumbe mzito kwa nchi hiyo kupanua wigo wa ushirikiano na Tanzania katika maeneo ya kimkakati kama vile uwekezaji, biashara, utalii, miundombinu, afya na elimu.
Waziri Kombo alieleza kuwa jukumu kubwa la Serikali zote duniani hivi sasa ni kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi na zile zinazosimamia masuala ya uwekezaji ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hivyo ziara yake inalenga sio tu kushawishi kampuni zenye nguvu nchini Czech kwenda kuwekeza Tanzania bali pia kuharakisha ukamilishwaji wa makubaliano ambayo kwa namna moja au nyingine yanapunguza kasi ya uwekezaji na biashara baina ya mataifa hayo.
Kufuatia azma hiyo, Waziri Kombo na mwenyeji wake wamekubaliana kuharakisha uwekaji saini wa Mkataba wa Anga ili kuruhusu safari za ndege za moja kwa moja baina ya mataifa hayo kwa lengo la kupanua sekta ya utalii ambayo ni sekta muhimu kwa mapato ya Tanzania. Idadi ya watalii kutoka Czech imekuwa ikiongezeka kila mwaka huku nchi hiyo ikifanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii visiwani Zanzibar.
Mkataba mwngine muhimu katika kuchagiza biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo ni Mkataba wa Kuepuka Utozaji wa Kodi Mara mbili ambapo pande zote zilikiri kuwa mkataba huo umefikia hatua nzuri na masuala yaliyosalia yatakamilushwa ili uweze kusainiwa mapema mwaka huu.
Waziri Kombo amesema Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu na rasilimali za kutosha na kumuomba Waziri mwenzake awashawishi wafanyabiashara wengi wa Czech kuja kuwekeza Tanzania kama alivyo fanya mfanyabiashara mwenzao wa kampuni ya Airplanes Africa Limited kwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza ndege aina ya skyleader – 600 chenye makao makuu mkoani Morogoro.