Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesema nchi yake inaunga mkono mpango wa bara la Afrika kuwa na uwakilishi wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akiwa katika ziara ya siku mbili nchini Kenya, Scholz amemueleza Rais wa nchi hiyo William Ruto kwamba anaamini matatizo ya Afrika yatasuluhishwa kwa uongozi wa nchi za Afrika, akitoa mfano wa mapigano yanayoendelea nchini Sudan.
Aidha amesema, Ujerumani inaunga mkono wazo la Afrika kuwa mwanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na kupewa nafasi Umoja wa Afrika kuwa na mwakilishi kwenye kundi la nchi tajiri 20 duniani G-20.
Pendekezo la Umoja wa Afrika kuwa na nafasi katika mikutano ya nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi, G20 lilitolewa kwa mara ya kwanza na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Kabla ya ziara yake nchini Kenya iliyomalizika siku ya Alkhamisi, Kansela wa Ujerumani alitembelea Ethiopia na kufika makao makuu ya Umoja wa Afrika AU, ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Kamisheni ya umoja huo Moussa Faki Mahamat.
Wakati mabara ya Amerika, Ulaya na Asia yana nchi ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bara la Afrika ndilo pekee ambalo halina uwakilishi wa uanachama wa kudumu kwenye chombo hicho chenye sauti ya juu ndani ya umoja huo.