Leo April 19, 2018 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dr. Hamisi Kigwangalla amesema serikali imefanikiwa kudhibiti vitendo vya ujangili hapa nchini kwa zaidi ya asilimia 50.
Amezungumza hayo akiwa katika maongezi na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma.
Dk. Kigwangalla amesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa na kwamba nyara zinazokamatwa hivi sasa ikiwemo meno ya tembo na ngozi za wanyamapori ni masalia ya zamani.
“Mafanikio yametokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kudhibiti vitendo vya ujangili ikiwemo doria za mara kwa mara za kiitelijensia ambazo zimekuwa zikishirikisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama pamoja na raia wema.” -Kigwangalla
Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla amemueleza balozi Cooke kuwa, Serikali kupitia Wizara yake inaendelea kuimarisha vivutio vya utalii hapa nchini kwa kupanua jeografia ya maeneo ya utalii sambamba na kuongeza vivutio ili kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Amesema Serikali itajenga makumbusho ya Marais Wastaafu wa Tanzania mjini Dodoma pamoja na kuanzisha makumbusho ya meno ya tembo katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Iringa na Dodoma.
Amesema Serikali pia itaanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Uendelezaji wa Fukwe nchini ili kuimarisha utalii wa fukwe pamoja na kutambua barabara iliyokuwa ikitumika katika biashara ya utumwa wakati wa ukoloni ili iweze kutumika kiutalii.
Nae balozi Cooke amesema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kudhibiti mtandao wa uhalifu wa madawa ya kulevya, rushwa na ujangili.
“Watalii zaidi ya 75,000 wa Uingereza hutembelea Tanzania kila mwaka na wengine wamewekeza katika sekta utalii hapa nchini, hivyo naiomba Serikali kurekebisha baadhi ya changamoto chache zilizopo katika sekta hiyo kwenye mtiririko wa kodi.” -Cooke