Katika matamshi yake ya kwanza binafsi, Mkurugenzi wa Shirika la Afya duniani, WHO, Tedros Ghebreyesus, ameeleza maumivu aliyonayo kuhusu mzozo unaoendelea nchini mwake Ethiopia, kuhusu eneo la Tigray.
“Ukiachilia ugonjwa wa Covid 19, mwaka 2020 umekuwa mgumu sana kwangu sababu nchi yangu ina matatizo,” amesema Tedros wakati alipozungumza na waandishi wa habari wiki hii.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiyi Ahmed, ambaye mwaka jana alishinda tuzo ya amani ya Nobel, aliagiza wanajeshi kuvamia mji wa Kaskazini mwa nchi hiyo Tigray Novemba 4, akidai operesheni iliyofanyika ni kujibu mashambulizi ya kambi ya wanajeshi wa Serikali, yaliyofanywa na wapiganaji wa Chama cha TPLF, kinachoongoza eneo hilo.
Mapigano hayo kwenye mji wa Tigray, yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha hii ni kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya mizozo, huku maelfu wengine wakikimbilia nchi jirani kuwa wakimbizi.