Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Chakula duniani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa vyakula kuandaa vyakula katika hali salama yakiwemo mazingira salama ili kuweza kumlinda mlaji asiweze kupata madhara ya kiafya.
Kauli mbiu ya mwaka huu kuelekea Siku ya Usalama wa Chakula ambayo huadhimishwa kila mwaka June 7 ni “Chakula Salama kwa Afya njema ya kesho”.
Ameyasema hayo Afisa Usalama wa Chakula Mwandamizi wa TBS, Imakulata Justin akizungumza kuelekea Siku ya Chakula Salama Duniani, katika ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini DSM Imakulata amesema mazingira ya pale wanapozalisha vyakula kunahitajika kuwa safi na salama ili kuhakikisha kile chakula kinachozalishwa ni salama.
“Unapofanya biashara ya chakula basi unatakiwa kuhakikisha chakula hicho kinakuwa katika hali ambayo haiatarishi usalama wa chakula husika mfano kuna chakula kinatakiwa kuwekwa kwenye hali ya ubaridi basi kiwekwe hivyo au kinatakiwa kuhifadhiwa katika sehemu kavu basi kifanyiwe hivyo” Imakulata.
Pamoja na hayo amesema jukumu la TBS ni kuhakikisha chakula kinachozunguka katika masoko ni salama hivyo hufanya kaguzi mbalimbali katika masoko kuhakikisha kwamba kile kinachouzwa ni salama kwaajili ya afya ya mlaji.