Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, watu karibu 85,000 wamekimbia mapigano katika eneo la Masisi, mkoa wa Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuanzia Oktoba Mosi, na kufanya jumla ya watu waliokimbia makazi yao mkoani humo kufikia zaidi ya milioni mbili.
Wakimbizi wa hivi karibuni wametafuta hifadhi katika maeneo salama, ikiwemo sehemu nyingine za eneo la Masisi na eneo la Rutshuru, ambako wamepewa hifadhi katika vituo vya pamoja, na kuongeza kuwa, wengi wao wanaishi katika mazingira duni.\
Ofisi hiyo imeripoti kuwa mapigano yamefunga barabara kati ya mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, na mji wa Kitshanga katika eneo la Rutshuru, na kusababisha mashirika mengi ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kusitisha operesheni zao katika eneo la Kitshanga na maeneo jirani.