Hali mbaya ya hewa imesababisha vifo vya watu milioni 2 na uharibifu wa kiuchumi wa dola trilioni 4.3 katika kipindi cha nusu karne iliyopita, ripoti ya Umoja wa Mataifa imegundua.
Kulingana na takwimu mpya zilizochapishwa Jumatatu kutoka Shirika la Hali ya Hewa Duniani la Umoja wa Mataifa (WMO), majanga 11,778 yanayohusiana na hali ya hewa yametokea kutoka 1970 hadi 2021, na yameongezeka katika kipindi hicho.
Ripoti hiyo imebaini kuwa zaidi ya asilimia 90 ya vifo vilivyoripotiwa duniani kote kutokana na majanga hayo vimetokea kwenye nchi maskini na zinazoendelea.
Mkuu wa shirika linaloshughulikia hali ya hewa la Umoja wa Mataifa, (WMO), Petteri Taalas amesema katika taarifa yake kwamba: Kimbunga Mocha, ambacho kilisababisha maafa nchini Myanmar na Bangladesh wiki iliyopita, ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo.
Lakini WMO pia imesema, kuboreshwa mifumo kutoa tahadhari ya mapema na kuratibu usimamiaji wa maafa kumepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya binadamu.
Amesema wakati majanga kama ya kimbunga cha Mocha yalipotokea huko nyuma huko “Myanmar na Bangladesh yalisababisha vifo vya makumi bali hata mamia ya maelfu ya watu, lakini hatua zilizochukuliwa baadaye kimataifa, zinaonekana kupunguza idadi ya vifo katika majanga kama hayo.
Katika ripoti yake ya mwaka 2021 iliyoangazia vifo na hasara zilizotokana na maafa ya kibinadamu tangu 1970 hadi 2019, shirika hilo lilisema kwamba mwanzoni mwa kipindi hicho, ulimwengu ulishuhudia vifo zaidi ya 50,000 kila mwaka lakini ilipofikia miaka ya 2010, idadi ya vifo vya maafa ilipungua na kufikia chini ya 20,000 kila mwaka.
Umoja wa Mataifa umezindua mpango wa kuhakikisha mataifa yote yanatumia mifumo ya tahadhari ya mapema ya majanga ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027. Hadi hivi sasa lakini, ni nusu tu ya nchi za dunia ndizo zilizo na mifumo hiyo.