Umoja wa Afrika umelaani vikali shambulio la anga lililofanywa na jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya hospitali ya Al Ahli Arab katika Ukanda wa Gaza hapo jana na kuua mamia ya watu.
Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU huku akieleza kusikitishwa na jinai hiyo ya Wazayuni amesema katika taarifa kuwa, “Hakuna maneno yanayoweza kutosheleza kueleza namna tunavyolaani shambulio la bomu la Israel dhidi ya hospitali Gaza.”
Mahamat ameeleza kuwa, kushambulia hospitali, ambayo inatazamwa kuwa kimbilio salama katika Sheria za Kimataifa za Ubinadamu, ni jinai ya kivita.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapasa kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na jinai hizo hivi sasa.
Wakati huohuo, Waziri wa Afya wa Djibouti, Ahmed Robleh Abdilleh amelaani shambulio hilo la kikatili na kueleza kuwa, kushambulia hospitali kwa kutumia silaha iliyopigwa marufuku ya fosforasi ni mauaji ya kimbari.
Waziri huyo wa Djibouti ameeleza bayana kuwa: Mashambulio ya mabomu ya namna hiyo hayawezi kukata kiu ya Wapalestina ya kupigania uhuru wao.