Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kupatikana kiasi dola bilioni sita ili kutoa msaada unaohitajika mno kwa watu wa Sudan, wakati nchi hiyo ikikabiliwa na hali mbaya.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu OCHA na lile la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, yamesema lengo la wito huo ni kupata fedha zitakazowezesha kutoa msaada kwa karibu watu milioni 26 katika mwaka huu wa 2025.
Tangu Aprili mwaka 2023, Sudan imetumbukia katika mzozo wa kikatili kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, anayeongoza Kikosi cha RSF.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vimewakosesha makazi watu milioni 12, wakiwemo karibu milioni 3.5 ambao wameikimbia nchi. Wakati huo huo, karibu theluthi mbili ya wakazi wa Sudan wanahitaji msaada wa dharura, huku maeneo mengi ya taifa hilo yakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.