Jumatatu hii, Desemba 11, Umoja wa Mataifa ulizindua ombi la michango yenye thamani ya dola bilioni 46.4 kwa mwaka wa 2024, ili kusaidia watu milioni 180.5 duniani. Bila ufadhili wa kutosha, “watu watakabiliwa na hali ngumu”, umeonya Umoja wa Mataifa, ambao unaangazia kuongezeka kwa migogoro, dharura ya tabi nchi au hata kuporomoka kwa uchumi, linaripoti shirika la habari la AFP.
Wito wa michango unalenga kufadhili shughuli katika nchi 72: nchi 26 zilizo katika mgogoro na nchi 46 jirani ambazo zinakabiliwa na athari, kama vile wimbi la wakimbizi. Nchi inayoongiza ni Syria (dola bilioni 4.4), ikifuatiwa na Ukraine (bilioni 3.1), Afghanistan (bilioni 3), Ethiopia (bilioni 2.9), na Yemen (bilioni 2.8).
Kunaweza kuwa na karibu watu milioni 300 wanaohitaji msaada ulimwenguni kote mnamo 2024, kulingana na Martin Griffiths. Lakini Umoja wa Mataifa utaelekeza nguvu zake tu kwa milioni watu 180.5 kati yao, wengine pia wanaweza kupata usaidizi kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika mengine pamoja na nchi zenyewe.
Iwapo macho yote kwa sasa yanaelekezwa katika vita vya Ukanda wa Gaza, Umoja wa Mataifa unakumbusha kuwa Mashariki ya Kati, Sudan na Afghanistan pia zimenufaika na oparesheni muhimu za misaada ya kimataifa. Hata hivyo, ukubwa wa wito wa kila mwaka na idadi ya walengwa ambao Umoja wa Mataifa unataka kusaidia imepunguzwa ikilinganishwa na mwaka 2023, kutokana na michango michache.
“Wasaidizi wa kibinadamu wanaokoa maisha ya watu, wanapambana na njaa, wanalinda watoto, wanakabiliana na milipuko ya magonjwa, na kutoa makazi na usafi wa mazingira katika hali zisizo za kibinadamu,” mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths, amesema katika taarifa yake. “Lakini msaada unaohitajika kutoka kwa jumuiya ya kimataifa haukidhi mahitaji,” amelaumu.