Taarifa ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuhusu kuongezeka kwa wasiwasi wa ukosefu wa chakula katika nchi za ukanda wa Sahel na viwango vya janga la njaa hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ya Burkina Faso na Mali ambako utoaji misaada ya kibinadamu unatatizwa pakubwa na ukosefu wa usalama.
Ripoti hiyo ilibaini kuwa, athari za pamoja za migogoro, majanga ya tabianchi, COVID-19 na bei ya juu ya vyakula zinaendelea kuzidisha njaa na utapiamlo katika eneo hilo.
Idadi ya watu ambao mara kwa mara hukumbwa na tatizo la uhaba wa chakula salama na chenye lishe bora inatarajiwa kufikia milioni 48 katika msimu wa kuanzia Juni hadi Agosti 2023 ikiwa ni ongezeko mara nne katika miaka mitano iliyopita.
Hivi karibuni ripoti mpya iliyochapishwa na taasisi moja inayofuatilia mashambulizi na mienendo ya makundi ya kigaidi duniani ilisema kuwa, vifo vinavyotokana na hujuma za kigaidi katika eneo la Sahel barani Afrika vimeongezeka kwa asilimia 2000 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.
Ripoti hiyo iliyochapishwa na taasisi ya Institute for Economics and Peace yenye makao yake Australia imeeleza kuwa, eneo la Sahel katika chini ya jangwa la Sahara barani Afrika ndicho kitovu cha ugaidi hivi sasa duniani.
Ukosefu wa uhakika wa chakula unaelekea kufikia kiwango cha juu zaidi katika miaka 10 katika Afrika Magharibi na Kati ifikapo Juni.