Umoja wa Mataifa umetia saini makubaliano na serikali ya Ghana na kuahidi kuipa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, dola milioni 500 za Kimarekani katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kuisaidia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Ghana Charles Abani amesema katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo kwamba, mkataba huo ni chombo muhimu zaidi cha kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo za Umoja wa Mataifa nchini Ghana na umeonyesha dhamira ya umoja huo ya kusimama bega kwa bega na Ghana katika kufanikisha ndoto zake za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs.
Amesema, msaada huo mpya utawezesha taasisi na watu kujenga uwezo wao katika maeneo matatu muhimu.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa ufafanuzi zaidi akisema “Maeneo hayo matatu muhimu ni mageuzi ya kiuchumi jumuishi, upatikanaji sawa wa huduma za msingi za kijamii na amani na usalama wa kudumu nchini Ghana na katika eneo hilo zima.”
Kwa upande wake, Mohammed Amin Adam, waziri wa nchi katika Wizara ya Fedha ya Ghana amesisitiza kuwa, msaada huo wa Umoja wa Mataifa ni uthibitisho mkubwa zaidi wa kwamba chombo hicho kikubwa zaidi ya kimataifa kiko bega kwa bega na wananchi wa Ghanda katika safari yao ya kujiletea maendeleo endelevu.
Mkataba huo utaongeza zaidi uwezo wetu wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs na kutuwezesha kufikia ajenda ya mabadiliko iliyoainishwa na serikali.