Umoja wa Mataifa umeitaka jamii ya kimataifa kutowasahau raia wanaokabiliwa na vita nchini Sudan, na kutoa wito wa ufadhili wa dola za kimarekani bilioni 4.1 ili kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu na pia kuwasaidia wakimbizi wa Sudan waliokimbilia nchi jirani.
Umoja huo umesema, karibu watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi nchini Sudan, huku zaidi ya watu milioni 1.5 wamekimbilia nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.
Katika taarifa yake ya pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetoa wito wa dola za kimarekani bilioni 2.7 kwa ajili ya kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu milioni 14.7.
Vita iliyodumu kwa miezi 10 kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha RSF imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, kutoa tahadhari ya janga la njaa, na kusababisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi hiyo.