Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa “ana wasiwasi sana” na hali mbaya ya maisha ambayo rais Mohamed Bazoum wa Niger na familia yake wanaripotiwa kuishi chini yake huku wakiendelea kuzuiliwa kiholela na wanachama wa Walinzi wa Rais nchini Niger.
Katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake Katibu Mkuu Antonio Guterres alitaka Bazoum “kuachiliwa mara moja bila masharti na kurejeshwa kama Mkuu wa Nchi.”
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, alisema kuwa Umoja wa Mataifa unafahamu ripoti kwamba Bazoum na familia yake wanaishi bila umeme, maji, chakula au dawa.
Rais aliyeondolewa madarakani wa Niger anakosa chakula na katika hali mbaya zaidi wiki mbili baada ya kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani, mshauri alisema Jumatano.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ilionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu “hali inayozidi kuzorota” ya kuzuiliwa kwake.
“Tunafahamu taarifa za hivi punde kwamba Rais Mohamed Bazoum wa Niger na familia yake wanaishi bila umeme, maji, chakula wala dawa, na ninaweza kusema yafuatayo: Katibu Mkuu anasikitishwa sana na hali mbaya ya maisha ambayo Rais Bazoum na familia yake inaripotiwa kuishi chini yake huku wakiendelea kuzuiliwa kiholela na wanachama wa Walinzi wa Rais nchini Niger.
Katibu Mkuu anasisitiza wasiwasi wake juu ya afya na usalama wa Rais na familia yake na kwa mara nyingine tena anatoa wito wa kuachiliwa mara moja, bila masharti na kurejeshwa kama Mkuu wa Nchi.
Katibu Mkuu pia amesikitishwa na ripoti zinazoendelea kuhusu kukamatwa kwa wanachama kadhaa wa serikali. Anatoa wito wa haraka wa kuachiliwa kwao bila masharti na ufuasi mkali wa majukumu ya kimataifa ya haki za binadamu ya Niger,” Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Rais Bazoum, kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia katika taifa hilo la Afrika Magharibi, amezuiliwa katika ikulu ya rais mjini Niamey akiwa na mkewe na mwanawe tangu wanajeshi walioasi walipomshambulia Julai 26.