Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afghanistan alionya watawala wa Taliban wa nchi hiyo Jumatano kwamba kutambuliwa kimataifa kama serikali halali ya nchi hiyo kutabaki kuwa “karibu haiwezekani” isipokuwa waondoe vikwazo vikali vya ukandamizaji wa haki za wanawake na wasichana ikiwemo elimu na ajira.
Roza Otunbayeva aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Taliban wameomba kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na mataifa mengine wanachama wake 192, “lakini wakati huo huo wanatenda kinyume na maadili muhimu yaliyoonyeshwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”
Katika majadiliano yake ya mara kwa mara na Taliban, alisema, “Sina ukweli kuhusu vikwazo walivyojitengenezea wenyewe kwa amri na vikwazo walivyoweka, hasa dhidi ya wanawake na wasichana.”
Kundi la Taliban lilichukua mamlaka nchini Afghanistan mwezi Agosti 2021 huku wanajeshi wa Marekani na NATO wakiwa katika wiki za mwisho za kuondoka nchini humo baada ya miongo miwili ya vita.
Amri za kundi hilo zinazozuia ushiriki wa wasichana na wanawake zimeathiri misaada ya kigeni kwa nchi hiyo, ambayo raia wake wanakabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani.
Taliban awali iliahidi sheria ya wastani zaidi kuliko wakati wao wa kwanza madarakani kutoka 1996 hadi 2001 lakini walianza kutekeleza vikwazo kwa wanawake na wasichana mara tu baada ya kuchukua 2021.
Wanawake wamezuiwa kufanya kazi nyingi na maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na bustani, bafu na kumbi za mazoezi, huku wasichana wakipigwa marufuku kupata elimu zaidi ya darasa la sita.