Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamenyamaza kwa dakika moja kuwaenzi zaidi ya wafanyakazi 100 waliouawa Gaza tangu vita vya Israel na Hamas kuanza mwezi uliopita.
Wafanyakazi katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva waliinamisha vichwa vyao na bendera kupepea nusu mlingoti huku mshumaa ukiwashwa kuwakumbuka wafanyakazi 101 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) waliouawa katika vita huko Gaza.
“Hii ni idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi wa misaada waliouawa katika historia ya shirika letu kwa muda mfupi,” alisema Tatiana Valovaya, mkurugenzi mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Geneva.
“Tumekusanyika hapa leo, tumeungana katika eneo hili la mfano, kutoa heshima kwa wenzetu jasiri waliojitolea maisha yao wakati wakihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa.”
UNRWA imesema baadhi ya wafanyakazi waliuawa wakiwa kwenye foleni ya kutafuta mkate, huku wengine wakiuawa pamoja na familia zao majumbani mwao katika vita vya anga na ardhini vya Israel dhidi ya Hamas.
“Ningependa kusema kwamba kwa kweli tunakabiliwa na nyakati zenye changamoto nyingi za ushirikiano wa kimataifa, kwa ulimwengu,” Bi Valovaya alisema. “Lakini Umoja wa Mataifa unafaa zaidi kuliko hapo awali.”