Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu hali mbaya ya Gaza na kusema: Vyumba vya kuhifadhia maiti vimejaa maiti na maeneo ya makazi raia yameharibiwa kabisa.
Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, amesema kuhusu hali ya sasa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu kwamba: “Hakuna umeme, maji wala nishati huko Gaza. Akiba ya chakula pia inaelekea kuisha.”
Griffiths ameongeza kuwa: Hospitali zimejaa wagonjwa na zinakabiliwa na uhaba wa dawa. Nyumba, shule, makazi, vituo vya afya na mahali pa ibada vinaendelea kushambuliwa vikali kwa mabomu ya Israel.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa: “Huko Gaza, kufuatia agizo lililotolewa na Israel la watu kuhama makazi yao, mamia ya maelfu ya familia zimeshambuliwa kwa mabomu zikielekea kusini kwenye barabara zilizojaa na kuharibika, lakini hazikuwa na pa kwenda.”
Griffiths amesema karibu watu 2,000 wa Gaza wameuawa na idadi kubwa wamejeruhiwa, na kuongeza kuwa, maeneo yote ya makazi ya Gaza yameharibiwa na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wameuawa.