Siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kubatilisha hukumu ya Kifo na kuwa kifungo cha maisha jela, Umoja wa Mataifa umepongeza maamuzi ya Kenya juu ya kufuta adhabu ya kifo kwa maelfu ya watu waliokuwa wakisubiri kutekelezwa hukumu hiyo dhidi yao.
Kwa mujibu wa msemaji wa wa idara ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani, amesema hatua hiyo ya serikali ya Kenya ni ya kupongezwa, yenye kutia matumaini na inayofaa kufuatwa na nchi nyingine. Ravina amesema anaamini kuwa serikali ya Kenya itafanya mikakati ili kuhakikisha kuwa hukumu hiyo inafutwa kabisa kwa misingi ya sheria na katiba.
Rais Uhuru Kenyatta, Jumatatu iliyopita alibadili hukumu zote za kifo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kuzifanya kuwa kifungo cha maisha jela. Hatua hiyo imewaondolea adhabu ya kifo wafungwa 2,747 katika nchi hiyo ambayo haijamyonga mfungwa yeyote aliyehukumiwa kifo kwa kipindi cha miaka 30 mpaka sasa.
Kupunguzwa adhabu ya kifo kwa idadi kubwa ya wafungwa kulifanyika mara ya mwisho nchini Kenya mwaka 2009 wakati wa utawala wa Rais mtaafu Mwai Kibaki. Ripoti zimearifu kuwa, hukumu ya kifo ilitekelezwa mara ya mwisho nchini Kenya mwaka 1987.
ULIPITWA NA ALICHOONGEA MISS TANZANIA NO. 2 KUHUSU MSHINDI WA KWANZA? TAZAMA HAPA