Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limefichua kuwa, mtoto mmoja kati ya kila watoto wawili wakimbiza ana utapiamlo nchini Ethiopia.
Katika ripoti yake ya karibuni kabisa iliyosambazwa jana Alkhamisi, UNHCR imesema kuwa, kuna nakisi kubwa katika utoaji wa huduma za lishe kwa wakimbizi nchini Ethiopia na kwamba utafiti wa shirika hilo uliofanywa kwenye kambi na maeneo 21 kote Ethiopia unaonesha kuwa, mtoto mmoja kati ya kila watoto wawili wakimbizi, wenye umri wa hadi miaka 6 anasumbuliwa na utapiamlo.
Takwimu kutoka UNHCR zinaonesha kuwa takriban watoto 95,334 kati ya 203,371 (laki mbili na 3371), ikiwa ni asilimia 46.9 ya watoto hao wakimbizi wamegundulika kuwa na matatizo ya utapiamlo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miongoni mwa matatizo ya watoto hao ni pamoja na kudumaa, uzito mdogo na upungufu wa virutubishi.