Kamishna wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Filippo Grandi ameisifu Ethiopia kwa sera yake ya kufungua mlango na huduma kwa wakimbizi.
Grandi ametoa pongezi hizo alipokutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Demeke Mekonnen mjini New York, Marekani, kando ya Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema katika taarifa yake kuwa, Bw. Grandi ameisifu nchi hiyo kwa kupokea na kuwahudumia wakimbizi wa Sudan kwa ukarimu na kwa njia ya kibinadamu. Pia Bw. Grandi ametoa wito kwa wafadhili kuongeza uungaji mkono kwa wakimbizi walioko nchini Ethiopia.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), kutokana na hali mbaya ya usalama nchini Sudan, idadi ya watu wanaoingia nchini Ethiopia kutokea Sudan imefikia 78,598 mpaka mwisho wa mwezi uliopita.