Mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na kimbunga Yagi yamewaacha karibu watoto milioni sita kote Kusini-mashariki mwa Asia wakihangaika kupata maji safi, chakula, na makazi, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto.
Dhoruba kali zaidi kuwahi kukumba eneo hilo mwaka huu, Yagi ilipiga Ufilipino mapema Septemba kabla ya kusababisha uharibifu kote Vietnam, Thailand, Laos na Myanmar.
Zaidi ya watu 500 wameuawa – karibu 300 nchini Vietnam, kadhaa nchini Thailand na angalau 236 nchini Myanmar. Mamilioni ya watu huko tayari wamehamishwa na vita.
“Watoto na familia zilizo katika mazingira magumu zaidi zinakabiliwa na matokeo mabaya zaidi ya uharibifu ulioachwa nyuma na Kimbunga Yagi,” June Kunugi, mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Asia Mashariki na Pasifiki, alisema katika taarifa Jumatano. “Kipaumbele cha haraka lazima kiwe kurejesha huduma muhimu ambazo watoto na familia zinategemea sana, ikiwa ni pamoja na maji safi, elimu na afya.
Ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa katika Kusini-mashariki mwa Asia, yanayochochewa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa, ni ukumbusho wa kusikitisha kwamba wakati misiba inapotokea, watoto walio katika mazingira magumu mara nyingi hulipa gharama kubwa zaidi.”
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya kibinadamu limesema kuna uhitaji wa dharura wa chakula, maji ya kunywa, dawa, nguo na malazi kwa wale walioathiriwa na mafuriko.