Uhuru wa vyombo vya habari uko hatarini katika kila kona ya dunia, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa alisema Jumanne, akilaani mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari na usambazaji wa habari za uongo.
Akizungumza siku moja kabla ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo ni leo Jumatano, Antonio Guterres aliwasilisha malalamiko kwa niaba ya waandishi wa habari na vyombo vya habari kote ulimwenguni.
“Uhuru wetu wote unategemea uhuru wa vyombo vya habari,” alisema kupitia ujumbe wa video, akiutaja kuwa msingi wa demokrasia na haki” na uhai wa haki za binadamu.”
“Lakini katika kila kona ya dunia, uhuru wa vyombo vya habari uko hatarini,” Guterres aliongeza, akihutubia mkutano uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New York.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa hakutaja majina ya waandishi wa habari waliofungwa jela au kutoa lawama kwa nchi, lakini wazungumzaji wengine waliangazia kesi binafsi, kama ile ya mwandishi wa habari wa gazeti la Wall Street Journal Evan Gershkovich anayezuiliwa Russia kwa tuhuma za ujasusi, ambazo anakanusha.
“Vita vya uhuru wa vyombo vya habari, vita vya kuachiliwa kwa Evan ni vita vya uhuru wa kila mtu, mchapishaji wa Wall Street Journal Almar Latour aliliambia kongamano hilo.
Takriban wafanyikazi 67 wa vyombo vya habari waliuawa mnamo 2022 – ongezeko kubwa la asilimia 50 kuliko mwaka uliopita. Takriban robo tatu ya waandishi wa habari wa kike wamenyanyaswa mtandaoni, na mmoja kati ya wanne ametishiwa kimwili.
Miaka kumi iliyopita, Umoja wa Mataifa ulizindua Mpango wa Utekelezaji wa Usalama wa Wanahabari ili kuwalinda wafanyakazi wa vyombo vya habari na kukomesha kutokujali kwa uhalifu unaofanywa dhidi yao.
Katika siku hii na kila Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, dunia lazima izungumze kwa sauti moja.
Acha vitisho na mashambulizi.
Acha kuwafunga jela na kuwafunga waandishi wa habari kwa kufanya kazi zao.
Acha uongo na kupotosha.
Acha kulenga wasema ukweli
Wanahabari wanaposimamia ukweli, ulimwengu unasimama pamoja nao.Alisema.