Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeendelea kuandika historia katika matibabu ya kibingwa na kibobezi hapa nchini ambapo kwa mara ya kwanza imeanzisha huduma ya upasuaji wa mishipa ya mgongo kwa njia ya matundu (Neuro spine endoscopic surgery).
Huduma hiyo imeanzishwa kufuatia kongamano la kimataifa la madaktari bingwa wa ubongo na mgongo na mishipa ya fahamu (Global Neurosurgery course) ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya MOI na Chuo kikuu cha Weill Cornell cha Marekani ambapo ya timu ya wataalam 120 wanashiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI Prof. Abel Makubi amesema tayari wagonjwa 13 wa mgongo wamefanyiwa upasuaji kwa mafanikio makubwa katika siku mbili (Jumatano na Alhamisi) toka kuanza kwa huduma hiyo.
Amesema uanzishwaji wa huduma hiyo inayotumia teknolojia ya kisasa inayotawala dunia kwa sasa na itasaidia kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata matibabu ya aina hiyo nje ya nchi na kukuza tiba utalii hapa nchini.
“Hii ni kwa mara ya kwanza kwa MOI na ni mara ya kwanza kwa Taifa kufanya upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu (Neuro spine endoscopic surgery), kwa dhati tunakishukuru chuo kikuu cha Weill Cornel cha Marekani kwa ushirikiano huu muhimu na kwa niaba ya menejimenti naahidi tutauenzi” amesema Prof. Makubi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Mgongo kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornel Marekani Prof. Roger Hartl ameahidi kuendeleza ushirikiano na Taasisi ya MOI katika kuendelea kuwajengea uwezo wataalam, kuwezesha tafiti za kisayansi na vifaa tiba vya upasuaji ili iweze kuwa kituo mahiri cha upasuaji wa mgongo barani Afrika.
“Lengo letu kuiona MOI ikiwa kituo cha umahiri kwenye kutoa tiba na mafunzo kwa mataifa mengine juu ya upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu, nimefurahi kuona namna ambavyo MOI inathamini ushirikiano wetu na ninaahidi kuuendeleza” amesema Prof. Hartl