Upigaji kura kwa duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais nchini Chad utafanyika Mei 6, Tume Taifa ya Uchaguzi (ANGE) imetangaza siku ya Jumanne wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Uchaguzi wa urais nchini Chad utafanyika Mei 6, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (ANGE) imetangaza siku ya Jumanne, uchaguzi ambao utamaliza kipindi cha mpito kilichodumu kwa miaka mitatu. Mahamat Idriss Déby Itno alitangazwa kuwa rais wa kipindi cha mpito, akiwa mkuu wa utawala wa kijeshi unaoongozwa na majenerali 15, baada ya kifo cha baba yake Idriss Déby Itno, aliyejeruhiwa vibaya na waasi katika uwanja wa vita mnamo mwaka wa 2021.
Mara moja aliahidi kurudisha mamlaka kwa raia kwa kuandaa uchaguzi miezi 18 baadaye, tarehe ambayo hatimaye iliahirishwa kwa miaka miwili. Mwisho wa kipindi cha mpito nchini Chad uliahirishwa hadi Oktoba 10, 2024. “Mbali na tarehe hii (Oktoba 10), nchi itaanguka katika ombwe la kisheria, sawa na machafuko yanayotabirika. Kwa hivyo ni muhimu kudumisha uchaguzi kabla,” ametangaza mwenyekiti wa ANGE Ahmet Bartchiret.
“ANGE imeanzisha ratiba halisi na inayoweza kufikiwa ambayo imeundwa hasa katika mambo yafuatayo: Mei 6, 2024, kufanyika kwa duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais,” ametangaza Bw. Bartchiret. Rais Déby, hata hivyo, alitangaza mbele ya Umoja wa Afrika kkwamba hatagwania katika uchaguzi wa urais ujao, lakini katikati ya mwezi wa Desemba Katiba mpya iliyopitishwa na kura ya maoni hatimaye ilimruhusu kugombea.