Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa wito kwa wajasiriamali, wafanyabiashara na wananchi kutumia huduma ya upimaji wa sampuli kwa hiari kwa lengo la kujihakikishia ubora na usalama wa bidhaa wanazonunua kwa ajili ya matumizi binafsi ikiwa ni pamoja na matumizi katika miradi mbalimbali.
Wito huo umetolewa leo na Afisa udhibiti ubora Ibrahim Feruzi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.
Amesema huduma ya upimaji wa sampuli kwa hiari inamjengea imani mnunuzi wa bidhaa anazonunua kuwa ni bora kwa matumizi na zinakidhi matakwa na mahitaji yake.
Vilevile kupitia huduma hii itawafaidisha wadau kutopata hasara kwani watajiepusha na athari za kutumia bidhaa zilizo chini ya kiwango.
Kwa upande wa miradi kwa kutumia huduma hii wakandarasi wanakaribishwa kupima bidhaa zote za ujenzi hii itasaidia hususani kwenye suala la usalama kwani tunatambua kuna miradi mingi ya kimkakati na suala la ubora wa vifaa vya ujenzi linapewa kipaumbele.
TBS inawakaribisha wadau kutumia huduma ya upimaji bidhaa kwa hiari kwa manufaa ya kiuchumi na usalama kwani huduma hiyo ina umuhimu mkubwa katika nyanja hizo.