Wafanyabiashara Magdalena Uhwello na Halima Nsubuga wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka 7 ikiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha. Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai washitakiwa walitenda makosa hayo kati ya Aprili Mosi, 2017 na Juni 30, 2017.
Miongoni mwa mashitaka hayo inadaiwa Aprili Mosi, 2017 na Juni 30, 2017 maeneo ya jiji la Dar es Salaam washitakiwa hao walikula njama kutenda kosa la kusimamia na kuendesha biashara ya upatu.
Katika mashitaka ya utakatishaji fedha, Wakili Simon amedai Aprili Mosi, 2017 na Juni 30, 2017 washitakiwa hao walijihusisha na muamala wa Dola za Marekani Laki 394,265 kwenye akaunti ya Magdalena na Halima kupitia akaunti zao za Benki wakati wakijua kwamba fedha hizo ni zao la kosa la kuendesha biashara ya upatu.
Inadaiwa Aprili 22, 2017 maeneo ya jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kuficha chanzo halali cha fedha hizo, walihamisha Dola za Marekani 12,309 kwa Benki ya Equity Uganda kwa jina la Smart Magara.
Hakimu Simba alisema kwa mujibu wa sheria mashitaka wanayoshitakiwa hayo washitakiwa hao hayana dhamana kisheria hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 30, mwaka huu kwa ajili yakutajwa.