Shirika la nyuklia la serikali ya Russia, Rosatom, na Burkina Faso zimetangaza mpango wa ushirikiano katika sekta ya nyuklia.
Mapatano hayo yamefikiwa katika mkutano wa kimataifa wa teknolojia ya nyuklia wa Atomexpo 2024 wa siku mbili ambao ulianza jana katika mji wa Sirius katika Bahari Nyeusi.
Kikao hicho kimeleta pamoja maafisa wakuu kutoka nchi 75, zikiwemo Mali, Burkina Faso, Niger na Iraq, ambazo zilihudhuria Atomexpo kwa mara ya kwanza.
Waziri wa Nishati, Migodi na Machimbo wa Burkina Faso Yacouba Zabré Gouba ameliambia Shirika la Habari la Sputnik pembezoni mwa kongamano hilo kwamba: “Mpango huu wa ushirikiano na Rosatom una vipengele kadhaa. Kwanza, unahusu mafunzo, maoni ya umma na kisha ujenzi wa miundombinu.”
Waziri huyo ameendelea kusema kuwa, kwa mujibu wa mpango wa ushirikiano, Rosatom itajenga kinu cha nyuklia cha kuzalisha nishati nchini Burkina Faso.