Kremlin ilisema Jumanne kwamba haiwezekani kwa Urusi kurudi kwenye mpango wa uuzaji wa nafaka wa Bahari Nyeusi kwa sasa, kwani makubaliano yanayohusiana na masilahi ya Urusi “hayatekelezwi”.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari, hata hivyo, kwamba rais Vladimir Putin alikuwa ameweka wazi kwamba mpango huo unaweza kufufuliwa ikiwa sehemu inayoangazia Urusi ya makubaliano hayo itaheshimiwa, Reuters inaripoti.
Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki Julai mwaka jana, yalilenga kusaidia kuzuia mzozo wa chakula duniani kwa kuruhusu nafaka zilizozuiliwa na mzozo wa Ukraine kusafirishwa nje kwa usalama.
Peskov alisema itakuwa muhimu kwa Urusi kujadili usambazaji wa nafaka na nchi za Afrika katika mkutano wa kilele wa Russia na Afrika baadaye wiki hii.