Mahakama ya juu ya Urusi imeamua kwamba moja kati ya mashirika maarufu ya haki za binaadamu nchini humo la Memorial, lifungwe kwa kuvunja sheria zinazohitaji mashirika kama hayo kujisajili kama mawakala wa mashirika ya kigeni.
Uamuzi huo unatokea katikati ya matukio ya ukandamizaji dhidi ya upinzani na makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo.
Ukandamizaji huo umeshuhudia pia kutiwa gerezani kwa mkosoaji mkuu wa Kremlin, Alexei Navalny. Hata hivyo, serikali ya Urusi inasema inatekeleza sheria za kuzuia itikadi kali na kujikinga dhidi ya ushawishi wa kigeni.
Shirika la habari la Interfax limemnukuu wakili wa shirika hilo la Memorial akisema, kufungwa kwa shirika hilo kumechochewa kisiasa na kwamba watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo nchini Urusi na pia katika mahakama ya Ulaya ya haki za binaadamu.