Mwanaharakati wa Ukraine amehukumiwa kifungo cha miaka 18 jela na mahakama ya kijeshi ya Urusi kwa kujaribu kulipua majengo katika mji unaokaliwa wa Melitopol.
Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilisema Dmitri Golubev alipatikana na hatia ya “ugaidi wa kimataifa” baada ya kutekeleza mlipuko mmoja katika makao makuu ya polisi wa trafiki mnamo Agosti mwaka jana na kupanga njama zingine mbili.
“Mimi ni Mukreni, nilikuwa nikiitetea Ukraine,” Golubev alinukuliwa na gazeti la Urusi la Kommersant akiiambia mahakama.
Waendesha mashtaka walisema mwanaharakati huyo alifunzwa na kupewa vifaa na huduma za siri za Ukraine.
Mji wa kusini mwa Ukraine wa Melitopol ulitekwa na jeshi la Urusi katika wiki ya kwanza ya uvamizi wao mnamo Februari 2022.