Maadhimisho ya utalii wa Maporomoko ya Maji Duniani yaani “International Waterfalls Day” yatakuwa JUNE 16, 2024 Duniani kote ambapo kwa Tanzania yatafanyika Nyanda za Juu Kusini katika mikoa ya Njombe na Mbeya – Hifadhi ya Mpanga Kipengere.
Hifadhi ya Mpanga Kipengere iliyo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa Mwaka huu, 2024imeyapa HADHI MAALUM maadhimisho hayo inayofahamika kama “Waterfalls Royal Tour” ikilenga kuendeleza jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassankatika ukuzaji wa Utalii nchini.
Hifadhi imekuja na USIKU WA KUSINI ili kuwezesha watalii kutumia muda mrefu zaidi hifadhini siku ya kilele kufurahia TUNUhiyo ya Maporomoko ya Maji yanayopatikana kwa wingi Nyanda za Juu Kusini pekee; yakiwepo ya Kimani, Merere, Nyaugenge na Idzumbo pamoja na utalii wa HIMAYA ya Chifu Mkwawa ndani ya Hifadhi.
Vilevile, usiku huo utazileta pamoja tamaduni zote za Nyanda za Kusiniikijumuisha vyakula, ngoma, vinywaji vyao vya asili pamoja na mila na desturi za watu wa Nyanda za Juu Kusini. Pia kutakuwa na nyamapori choma, supu ya uyoga, sinema na mziki mzuri wa nyikani, katika kambi ya utalii ya Kimani; ambapo mtalii atakuwa akipata mikito na mirindimo ya maji ya Maporomoko ya Kimani na upepo mwanana wa mbugani.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Maporomoko ya Maji kwa mwaka huu: Maporomoko ya Maji ni MAISHA na NISHATI.