Kampuni ya Geita Gold Mining Limited imeibuka mshindi katika vipengele vitatu muhimu na mshindi wa jumla wa kampuni inayofanya vizuri katika sekta ya madini mwaka 2019/2020.
Tuzo hizo zimetolewa na Serikali kwenye mkutano wa kila mwaka wa madini na uwekezaji katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, ambalo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu, GGML imetambuliwa kwa mchango wake katika sekta ya madini na ukusanyaji wa mapato ya serikali, utendaji mzuri katika masuala ya mazingira na usalama sanjari na utekelezaji mzuri wa miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii kwa mwaka 2019/2020.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hizo, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo ameishukuru serikali kwa kutambua mchango wa GGML na kuahidi kuendelea kufanya kazi na wadau wote katika sekta ya madini ili kufikia malengo ya Serikali ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa.
“Kuibuka mshindi katika vipengele vya kodi, mazingira na usalama sanjari na utekelezaji mzuri wa miradi kwenye jamii inayotuzunguka ni ushuhuda wa dira ya Kampuni yetu ambayo ni kuwa Kampuni ya kwanza ya madini duniani. Tuzo hizi zinatambua pia mchango wetu kama washirika muhimu wa maendeleo kwenye Serikali ya Tanzania pamoja na tunu zetu muhimu za kuhakikisha jamii inayozunguka Mgodi inafaidika kutokana na shughuli zetu,” Shayo.
“Kwa miaka 21 iliyopita, kampuni ya GGML imekuwa mshirika muhimu wa kusaidia jitihada za serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya madini ikiwemo michakato ya kushirikiana na kujadiliana ambayo imekuwa ikichochewa na Wizara ya Madini,” Shayo
Amesema GGML itaendelea kufanya kazi na Serikali ili kufikia malengo ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya madini inachangia zaidi ya asilimia 10 ya pato ghafi la taifa ifikapo Mwaka 2025.
Mwaka huu GGML walikuwa mojawapo pia ya wadhamini wakuu wa mkutano huo wa siku mbili ambao umemalizika 23 Februari 2021.