Siku si nyingi kuanzia sasa klabu ya Barcelona itakuwa na uongozi mpya ambao utaingia madarakani kuelekea mwishoni mwa msimu huu wakati ambapo klabu hii itafanya uchaguzi wake mkuu .
Hii ni baada ya Rais Jose Maria Bartomeu kutangaza kuwa klabu hii itafanya uchaguzi wake mwaka huu akisogeza mbele uchaguzi huo ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika mwaka 2016.
Hii ni kutokana na shinikizo kubwa ambalo amepata toka kwa wanachama wa klabu hiyo ambao wanafahamu kiini cha migogoro inayoendelea sasa kuwa uongozi mbovu uliokuwepo kwenye klabu hiyo chini ya rais wa awali Sandro Rosell ambaye alijiuzulu mwaka jana.
Moja kati ya majina mabayo yamekuwa yakitajwa kuhusika na uongozi mpya ni rais wa zamani Joan Laporta ambaye amekuwa akisema wazi kuwa anataka kurudi kuongoza klabu hiyo .
Laporta hata hivyo hatakuwa kwenye nafasi ya faida kama uchaguzi huo utafanyika mwaka huu kwani atakosa muda wa kujipanga kama ambavyo ingekuwa kama uchaguzi ungefanyika mwakani.
Pamoja na hayo bado Laporta anapewa nafasi kubwa ya kuchukua kiti cha urais endapo atatangaza kugombea.
Tayari Laporta ameshaweka mipango ya uongozi mpya wa timu hiyo kuanzia kwenye benchi la ufundi ambako amezungumza na kocha wa zamani wa Barca Pep Guardiola ambaye amekubali kimsingi kurejea Barca katika nafasi ya Ukurgenzi wa Ufundi mara mkataba wake na Bayern Munich utakapomalizika .
Chini ya Guardiola Laporta amepanga kuwarejesha wachezaji wa zamani wa Barca ambao ni Carles Puyol na Eric Abidal kuwa wasaidizi wa kocha ambaye alipanga kumteua Xavi Hernandez ambaye anamalizia muda wake kama mchezaji huku akichukua kozi ya ukocha .
Hata hivyo kurudishwa nyuma kwa tarehe ya uchaguzi kumevuruga mipango ya Laporta kwani bado Xavi anacheza na hawezi kumaliza kozi ya ukocha mwaka huu huku kukiwa na tetesi za kurudishwa kwa kocha wa zamani Frank Rijkaard kufuatia ombi la Messi taarifa ambazo hata hivyo zimekanushwa vikali na Messi mwenyewe na rais wa klabu hiyo.