Kikosi tawala cha kijeshi nchini Mali siku ya Alhamisi kilipiga marufuku utangazaji wa vyombo vya habari vya vyama vya siasa siku moja baada ya kusimamisha shughuli zao, kuashiria ukandamizaji wa hivi punde dhidi ya upinzani katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Sauti za upinzani zimezimwa kwa kiasi kikubwa tangu kanali walipochukua mamlaka katika mapinduzi ya 2020, na kumpindua rais wa kiraia Ibrahim Boubacar Keita.
Mamlaka ya juu ya mawasiliano ya Mali ilitoa taarifa Alhamisi ikitoa wito kwa “vyombo vyote vya habari (redio, televisheni, vyombo vya habari vilivyoandikwa na mtandaoni) kusitisha utangazaji na uchapishaji wa shughuli za vyama vya siasa na shughuli za asili ya kisiasa ya vyama”.
Haikuonyesha kitakachotokea kwa mashirika ya vyombo vya habari ambayo hayakuzingatia marufuku hiyo.
Hatua hiyo inajiri baada ya mamlaka mnamo Jumatano kuamuru kusimamishwa kwa muda usiojulikana kwa shughuli zote za kisiasa, ikisema inahitajika kudumisha utulivu wa umma.
Msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga alilaumu kusimamishwa kwa shughuli za chama kutokana na “majadiliano tasa” wakati wa jaribio la mazungumzo ya kitaifa mapema mwaka huu.