Jumuiya ya Umoja Wanawake (UWT) imechangia vifaa maalum katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wajawazito na ambao wameshajifungua.
Miongoni mwa vifaa hivyo ni pamoja na Mashine ya kupimia presha,kanga, nepi, sabuni za kuogea, na taulo za kike.
Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Azzan Zungu amepongeza jumuiya ya wanawake hao kwa kuonyesha namna taifa lilivyo na umoja, msimamo na upendo mmoja juu ya kuzidi kupenda na Kusaidiana.
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza dada zangu wa UWT Kariakoo pamoja na Gerezani awa ni vijana wadogo sana lakini wamemuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa huduma kwa jamii kuchangia vifaa vya kupimia presha,kisukari,nguo na vifaa mbalimbali kwa ajili ya wajawazito na wengine ambao tayari wameshajifungua huu ni upendo na umoja wa Taifa letu,” Amesema Zungu.
Naye Katibu UWT tawi la Kariakoo, Loema Joseph amesema wameamua kufanya hivyo ili kuwapa faraja wasijione wapo pekee yako hasa msimu huu wa sikukuu.
Hata hivyo kwa upande wake Daktari Hospitali ya Mnazi Mmoja, Faraja Ligate amewashukuru wanawake wa jumuiya hiyo kwa upendo walionyesha kwa kujali jamii yenye mahitaji.