Licha ya ongezeko la uzalishaji umeme kwa asilimia 14.2 katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, mwaka huu, serikali imesema bado kiwango hicho hakikidhi mahitaji ya taifa, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema hayo bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/25.
Katika makadirio hayo, Dk. Biteko ameliomba bunge kuidhinisha Sh. trilioni 1.883 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za wizara hiyo.
Biteko ametaja sababu zingine za upungufu wa umeme kuwa ni pamoja na upungufu wa maji na gesi asilia katika vituo vya kufua umeme, hitilafu katika mitambo ya uzalishaji na kufanyika kwa matengenezo katika mitambo ya uzalishaji wa nishati hiyo.
Amesema mahitaji ya juu ya umeme nchini yamekuwa na kufikia megawati 1,590.1 zilizofikiwa Machi 26, mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 8.1 ikilinganishwa na megawati 1,470.5 zilizofikiwa Juni 12, 2023.