Mazingira mazuri ya Uwekezaji na Biashara yaliyowekwa na Serikali, yamesaidia kampuni ya Lake Steel kuongeza uzalishaji na kuteka soko la nondo Nchini.
Mwenyekiti wa Kampuni za Lake Group, Bw. Ally Edha Awadh, ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa ofisi mpya ya Kampuni ya kuzalisha Nondo ya Lake Steel zilizopo katika jengo la Mwanga, Makumbusho Jijini Dar es Salaam.
Awadh amesema pamoja na uchanga wa Kampuni hiyo, imefanikiwa kuteka soko la nondo na ndiyo Kampuni inayohudumia karibu miradi yote ya kimkakati inajengwa na Serikali.
Mwenyekiti huyo ameipongeza Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kufungua uchumi ili kuruhusu uwekezaji zaidi ambao matokeo yake ni uzalishaji wa ajira nyingi hivyo ukuaji wa kasi wa uchumi.
Alisema kwa sasa wakati uhitaji umekuwa mkubwa kwenye soko kampuni inajiandaa kufunga mitambo mipya itakayoongeza uzalishaji wa nondo kutoka tani laki moja hadi kufikia tani laki moja na nusu ndani ya mwaka huu.
Meneja Mkuu, Bw. Ajay Jha, amesema hatua hiyo mpya ni ya kimkakati na itaongeza kasi ya biashara kwa kuwa wadau wengi wako karibu na ofisi mpya.
Meneja huyo amesema ofisi hiyo mpya inapatika katika Jengo la Mwanga Tower, ghorofa ya 17 lililo pembezoni mwa Barabara ya Bagamoyo, jijini Dar es Salaam.