Uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-salaam, leo tarehe 15 Mei, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema kuwa zoezi hilo litakapokamilika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638.
“Kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Daftari linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 hili ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa katika zoezi hilo wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.
Kuhusu idadi ya vituo, Jaji Mwambegele ameseama Tume ilifanya uhakiki wa vituo vya kuandikishia wapiga kura mwaka 2023 ambapo baada ya zoezi hilo iliamuliwa kuwa vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kwenye uboreshaji wa Daftari ni 40,126.
“Kabla ya uhakiki huo wa vituo, kulikuwa na vituo 37,814 ambavyo vilitumika kuandikisha wapiga kura mwaka 2019/2020. Baada ya zoezi hilo la uhakiki, jumla ya vituo 40,126 vitatumika kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari mwaka 2024/2025 ambapo kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar,” amesema Jaji Mwambegele.