Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dr Mwigulu Nchemba amewataka askari wa Jeshi la Magereza nchini kufanya kazi kwa weledi na kufata maadili ya kazi. Ameyasema hayo wakati akifungua gereza la wilaya ya chato mkoa wa Geita jana.
Waziri Dr Mwigulu amesema kuna taarifa ya baadhi ya askari wanaokiuka maadili ya kazi na masharti ya wahalifu wawapo magerezani kwa kushirikiana nao kwa kuwapa simu na vitu vingine ambavyo ni kinyume cha sheria na maadili ya kazi yao.
Dr Mwigulu ameongeza kusema kuwa kwasasa majira yamebadilika na aina ya wahalifu imebadilika hivyo ni wajibu wa askari kuzingatia maadili ya kazi zaidi kuliko walivyokuwa wakifanya zamani.
“Kuna taarifa kuwa baadhi ya maaskari wanawapa wafungwa simu ili wawasiliane na familia zao lakini kwasasa utakuta mfungwa amepewa simu kumbe anapanga mpango wa utekaji, majira yamebadilika hivyo tuzingatie sheria na maadili ya kazi zetu”. – Waziri Mwigulu
Naye Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Kamishna Jenerali Dk. Juma Malewa amesema kwasasa changamoto kubwa wanazokutana nazo ni pamoja na usafiri, upungufu wa askari hasa wanapofungua gereza jipya linahitaji askari wasiopungua 50 na changamoto nyingine ni miundombinu chakavu ya magereza na kumuomba waziri awasaidie kutatua changamoto hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Eng. Gabriel Robert amesema wao kama mkoa wamejipanga kutoa ardhi kwa jeshi la magereza kwa ajili ya kilimo na ufugaji ili waweze kujitegemea katika chakula na kiuchumi pale watakapo uza mazao watakayopata.
“Kama wewe ni Bodaboda, kuna haya ya kuzingatia” Waziri Mkuu