Staa wa Nigeria na klabu ya Napoli, Victor Osimhen sasa ameifikia rekodi ya lejendari wa Napoli, Muargentina Diego Maradona katika ufungaji wa mabao baada ya kufunga mabao 3 kwa mpigo usiku wa kuamkia leo.
Osimhen alikuwa moto wa kuotea mbali katika ushindi wa Napoli wa 6-1 dhidi ya Sassuolo kwenye Serie A Jumatano, Februari 28.
Nyota huyo wa Nigeria alifunga mabao yake mawili kati ya matatu katika kipindi cha kwanza, kabla ya kuifungia Napoli bao la tatu na kuufanya mpira kuwa wa kwake.
Osimhen amefunga katika kila mechi tangu arejee kutoka Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 akiwa na Nigeria. Super Eagles walipata kichapo kichungu kutoka kwa wenyeji Ivory Coast kwenye fainali.
Kwa hat trick yake, Osimhen alifunga mabao 11 katika Series A. Anajiunga na magwiji wa klabu Diego Maradona na Attila Salustro kama wachezaji pekee kufunga angalau mabao 10 ya Serie A katika misimu minne mfululizo, kwa mjibu wa jarida la Opta.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amefunga mabao 13 katika mashindano yote hadi sasa.
Msimu uliopita, alikuwa Mwafrika wa kwanza kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Serie A. Alifunga mabao 26 na kuisaidia Napoli kushinda taji lao la kwanza la ligi baada ya miaka 33. Amebakisha mechi 12 kufikia idadi hiyo msimu huu.