Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema haiutambui usajili wa Chuo cha Tanzania Aviation College kinachotoa mafunzo ya usafiri wa Anga chenye kampasi zake mikoa Mwanza, Dar es salaam na Arusha kwa kukiuka taratibu za uendeshaji wa Vyuo vya usafiri wa anga.
Hatua hiyo imekuja mara baada Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA) kufanya ukaguzi katika Chuo hicho Kampasi ya Mwanza na kujiridhisha kuwa kimekuwa kikitumia usajili namba CAA/ATO/050 ulioisha muda wake tangu mwaka 2018, ambapo kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za usajili kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Usafiri wa Anga, sura ya 80 na Kanuni zake.
Baada va Mamlaka kujiridhisha kuwa chuo tajwa hakijakidhi vigezo na hakitambuliki, hivyo mafunzo ya usafiri wa anga yanaendeshwa chuoni hapo kwa mgongo wa kutambulika na TCAA ni tendo ambacho ni kinyume na sheria lakini pia Wahitimu wa Chuo hicho wanakosa sifa za kupata leseni kutoka TCAA hivyo kushindwa kupata ajira.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imechukua maamuzi ya kukifungia Chuo hicho kuacha kutoa mafunzo yeyote yanayojihuisha na Usafiri wa Anga hadi pale watakapokidhi vigezo vyote vya Kisheria.
Itakumbukwa sep 30, 2020 Mamlaka ya usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilikifungia Chuo hicho kutokana kukiuka taratibu za usajili lakini Chuo hicho kimeendelea kutoa mafunzo kinyemela.