Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo ameongoza uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kumuwezesha Rais Samia kuchukua fomu ya kugombea Urais mwaka 2025, uchangishaji ambao umefanikisha kupatikana kwa shilingi milioni 120.
Wazo la kuchanga fedha hizo lilianzia kwa Mjasiriamali Mwanamke ambaye ni mmoja wa Wanawake waliohudhuria kongamano la leo lililokusanya Wanawake kutoka maeneo mbalimbali Tanzania katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es salaam, ambaye alisimama na kushukuru jinsi maisha yake yalivyobadilika chini ya Uongozi wa Rais Samia na kutoa shilingi elfu moja ya kumchangia Rais akachukue fomu.
“Kukajitokeza Mjasiriamali aliyeamua kumchangia Mh. Dr. Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu mwaka 2025 na akatoa shilingi elfu moja, wakinamama mliohudhuria hafla hii leo mliona kuwa shilingi elfu moja haitoshi kuchukua fomu na kumuunga mkono Mjasiriamali, Mama aliyewiwa kwa maendeleo yanayoletwa na Dr. Samia na kuongeza uchangiaji huo, naomba nitoe taarifa fedha ambayo imeratibiwa hapa na ile ambayo ilipatikana toka mwanzo imefanya kuwa na milioni 120, ndio mchango ambao kina Mama mmeweza kuchangia mchana huu” ——— alieleza Waziri Mkuu Majaliwa.