Oswald Kaijage (39) mkazi wa Buswelu Jijini Mwanza ambae ni Dereva wa gari aina ya Toyota Hilux Double cabin amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Ilemela na kufunguliwa Trafffic kesi namba 27 ya 2023 ikiwa ni pamoja na kusomewa shtaka moja lenye makosa 15 ikiwemo kusababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine tisa
Akisoma hati ya mashtaka August 01, 2023, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Anitha Mweli amesema Oswald anashtakiwa kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe na mwendokasi mkali na kusababisha vifo na madhara makubwa kinyume na Kifungu namba 40 (1), 63 (2) (a) na 27 (b) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002.
Hata hivyo mshtakiwa amekana kutenda makosa hayo huku Wakili wa Utetezi, Linus Amri akisaidiana na Steven Kitale wameiomba Mahakama hiyo kumpa dhamana mteja wao huku wakiainisha sababu tano za kuomba dhamana kwa mteja wao.
Baada ya kutaja sababu hizo Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Amani Sumari amesema makosa ya mshtakiwa huyo yanadhaminika na kumtaka awe na wadhamini wawili mmoja akiwa ni mtumishi wa Umma ambapo kila mmoja atasaini dhamana ya maneno ya fedha taslimu milioni 10.
Baada ya kukidhi masharti ya dhamana Hakimu Sumari amemuachia mshtakiwa kwa dhamana na kuahirisha shauri hilo hadi August 10, 2023 itakapoitwa kwa ajili ya kuanza usomwaji wa maelezo ya awali ya shtaka hilo.