Wakati Ukraine inadai kudhibiti maeneo 82 na 1,150 km² katika eneo la Kursk, Urusi itatuma vikosi vya ziada katika eneo la Belgorod, Waziri wa Ulinzi ametangaza siku ya Alhamisi, Agosti 15, siku ya tisa ya shambulio la Ukraine la kiwango ambacho hakijawahi kutokea.
Wakati wa mkutano unaohusu usalama wa maeneo ya mpakani, Andrei Beloussov ameripoti juu ya “mgao wa vikosi vya ziada na uwezo” katika mkoa wa Belgorod, jirani na ule wa Kursk, ambapo wanajeshi wa Ukraine walivamia mnamo Agosti 6.
Wakati huo huo Ukraine imeanzisha utawala wa kijeshi katika eneo la Urusi la Kursk. Kyiv imeanzisha utawala wa kijeshi katika eneo la Urusi la Kursk, eneo lilokumbwa na mashambulizi ya kushtukiza ya jeshi la Ukraine tangu Agosti 6, kamanda wa jeshi la Ukraine Oleksandr Syrsky ametangaza siku ya Alhamisi.
Urusi, kwa upande wake, itatuma vikosi vya ziada katika eneo la Belgorod, linalopakana na Ukraine, ametangaza Waziri wa Ulinzi wa Urusi.
Jeshi la Ukraine linatumia vifaru vilivyotolewa na Uingereza katika uvamizi wake wa ghafla katika eneo la Urusi, vyombo vya habari vya Uingereza vimesema siku ya Alhamisi.
Challenger 2 “ziliingia Urusi ili kushiriki katika shambulio la Ukraine huko Kursk,” kituo cha televisheni cha Sky News kimetangaza.
Magari haya ya kivita ya Uingereza yanatumiwa na askari wa Ukraine, inabainisha Sky, ambayo hata hivyo haijui ni ngapi ya magari haya ya kivita yako nchini Urusi.
Mshirika katika mstari wa mbele wa Kyiv, Uingereza ilikuwa nchi ya kwanza kupeleka magari ya kijeshi kwa Ukraine, ikiahidi 14 ya Challenger 2 zake kuanzia mwezi wa Januari 2023.