VIJANA 97,000 nchini wamenufaika mafunzo ya uanagenzi yanayotolewa kupitia programu ya kukuza ujuzi iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu inayolenga kufungua fursa nyingi za ajira kwa vijana.
Akizungumza jana jijini hapa namna Serikali inavyozalisha fursa za ajira, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi wa Ofisi hiyo, Ally Msaki alisema mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2017 kwenye vyuo vya ufundi 92 nchini na yanagharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo ni ya miezi sita na fani zinazotolewa ni ufundi umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, useremala, ufundi magari, umeme wa magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, utengenezaji wa vifaa vya aluminium, upishi, uhudumu wa hoteli na vinywaji, ushonaji, uchenjuaji wa madini, ufundi bomba, ufundi uashi, uwekaji wa terazo na marumaru, ufundi viyoyozi na majokofu.
Alifafanua kuwa kwa mwaka 2022/23 vijana 11,975 wanatarajia kupata mafunzona hadi kufikia Januari, 2023 vijana 7,760 wamepatiwa ujuzi huku wengine 4,215 wakitarajiwa kuanza mafunzo mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu.
Kadhalika Msaki alisema katika kuhakikisha vijana hao wanaunganishwa na mitaji kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana ili kujiajiri kwenye fani walizopata ujuzi.
“Kwa mwaka huu wa fedha 2022/23 tayari fedha Sh.Bilioni 1.5 zimeshakopwa na vijana waliomaliza mafunzo,”alisema. Hata hivyo, alisema ili kuwapatia vijana ujuzi wa kitaalaamu zaidi wameamua kufungua vituo atamizi katika mikoa minne ya Dar es salaam, Lindi, Singida na Kigoma.