Imeelezwa kuwa vijana wengi wanashindwa kupiga hatua za kiuchumi kutokana na kutokuwa na moyo wa uthubutu kwenye fursa za maendeleo ikiwemo ujasirimali na ubunifu wa miradi
Kwani licha ya serikali na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa vijana kundi kubwa lipo nyuma katika kupiga hatua kwa kisingizio cha mitaji jambo ambalo halina ukweli katika hatua za mwanzo za mafanikio.
Akizungumza wakati wa mkutano maalum uliwakutanisha vijana zaidi ya hamsini mwanzilishi wa taasisi ya Ubunifu (TAOTIC) yenye makao makuu yake Mkoa Morogoro Bwana Kiko Kiwanga amesema lengo la mafunzo hayo kuwainua vijana wa elimu ya juu, vyuo vikuu na wanaomaliza kwa lengo la kuwapa mbinu pamoja na mitaji itakayowawezesha kufikia malengo
Kiwanga amesema kuwa, vijana wengi wanamawazo pamoja na ndoto lakini wanakosa uelewa wa namna gani ya kuziendesha biashara zao hivyo kupitia Mradi wa AfriLabs wanatarajia kuwafikia vijana zaidi ya mia mbili
Kiwanga amesema TAOTIC kwa kushirikiana na AfriLabs wanaendelea kuwaunganisha vijana na wawekezaji mbalimbali pamoja na kuwapa mbinu ya utayari wa kupokea mitaji watakayopatiwa na wawekezaji.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wasema kuwa changamoto inayowakabili mpaka wanashindwa kufikia malengo ni kukosa mitaji hivyo wakipewa elimu ya kuongeza mawazo itawasaidia kufikia malengo hasa namna ya kupata mitaji.
Wanasema Licha ya serikali na wadau mbalimbali kutoa fedha na mitaji ili kuwainua kiuchumi lakini bado kundi hilo linakabiliwa na Ukosefu wa elimu ya biashara na ujasiriamali hivyo mafunzo hayo yatakuwa mkombozi kwa kuwainua kiuchumi.