Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) imeendelea kuhakikisha inaongeza thamani katika ardhi za Watanzania ambapo katika Wilaya ya Rorya, Mkoani Mara takribani vijiji 61 vitanufaika na mradi huo kwa kupangiwa matumizi ya ardhi ambapo mpaka sasa vijiji 40 matumizi yake yamekwishaandaliwa.
Mbali na mradi wa LTIP kupanga matumizi ya ardhi katika vijiji 61 wilayani humo, mradi utarasimisha mitaa 9 ambayo ni Obwere, Ngasaro, Kabwana, Oboke, Michire, Majengo, Utegi, Nyanchabakenye na Kirongwe.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) wilayani humo katika ukumbi wa Mapsap, tarehe 03 Aprili 2024 Mkoani Mara.
Amesema wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huo Wilayani Rorya ambapo uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji utasaidia kuainisha matumizi mbalimbali ya rasilimali ardhi kulingana na mahitaji.
‘‘Ongezeko la idadi ya watu limeongeza kasi ya ukuaji wa vijiji vyetu na baadhi ya vitovu vya vijiji kubadilika kuwa vijiji miji ambapo ukuaji huo umepelekea kuongezeka kwa migogoro ya ardhi, Ukuaji wa makazi yasiyopangwa, upungufu wa huduma za jamii na uharibifu wa mazingira hivyo mradi huu utasaidia kupunguza au kumaliza kabisa changamoto hizo’’ aliongeza Chikoka
Meneja Mradi Msaidizi kwa upande wa Vijiji Patrick Mwakilili amesema kuwa dhumuni la mradi huu ni kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kufahamu haki zao na kuongeza uelewa na umuhimu wa mwanamke kumiliki ardhi ikiwa ni pamoja na umiliki wa pamoja baina ya mume na mke na kuzingatia haki za makundi maalumu.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umedhamiria kutoa elimu kwa wadau katika ngazi ya Kitaifa, Wilaya, Mtaa/Kijiji mpaka Kitongoji ambapo kupitia Mkutano huo wa Wadau katika ngazi ya Wilaya wadau hupata fursa ya kutoa maoni yao ili kuboresha utekelezaji wa mradi katika maeneo yao.